Haki msingi wa amani, na haki ni kwa wote, kokote, bila ubaguzi

Dhana ya Msamaria Mwema niliyoitumia kuhitimisha makala yangu ya mwisho ni muhimu sana katika falsafa ya kisasa kwa maana kwamba inaelezea wema unaotendwa na mtu ambaye ndani ya jamii husika hatarajiwi kutenda wema. Msamaria Mwema aliyetolewa mfano na Bwana Yesu alikuwa mpita njia tu, kama walivyokuwa wapita njia wengine waliomkuta msafiri kapigwa, kaporwa na yu mahututi, mlangoni mwa kifo.

Walikwisha kupita watu wenye sifa za kutenda wema, wakiwemo makuhani, lakini wote walimuona mtu huyo kama mtu asiye na thamani, na wala hawakuona sababu ya kumsaidia. Hali yake ilikuwa haiwahusu, na ilibidi yeye mwenyewe apambane na hali yake, kama msemo wa siku hizi ulivyo. Msamaria akamuonea huruma mhanga yule, akamchukua, akampeleka hadi hospitalli, akamkabidhi kwa wauguzi na akalipia matunzo yake.

Ipo tofauti kubwa baina ya binadamu na mtu. Binadamu maana yake ni mwana wa Adamu na Hawa, kama ambavyo vitabu vya hekaya za Wayahudi zinavyoeleza. Sote tunachukuliwa kama watoto wa hao wawili waliokula lile tunda na, kutokana na kula lile tunda, wakatuachia changamoto za kila aina hadi leo hii. Mtu ni tofauti, kwa sababu pamoja na kuwa binadamu kwa maana niliyoeleza hapo juu, ana sifa ya nyongeza, kwa sababu yeye ana utu ndani yake.

Nakumbuka wimbo mmoja wa marehemu Marijani Rajabu ambamo anasema. ‘kwenye watu kumi, binadamu mmoja’. Niliwahi kumwambia mwanaziki huyo kuhusu kosa lake, lakini nilikubaliana naye kwamba ilikuwa haiwezekani kurekebisha kosa hilo, hasa kwa sababu halaiki ya wapenzi wa muziki walikwisha kulikubali kosa hilo kama sahihi.

Lakini uhalisia wa maneno hayo unatuambia kwamba ingawa wote waliopita na kumuona bwana yule amepigwa na kaumia walikuwa wote ni binadamu, aliyekuwa na UTU alikuwa ni mmoja peke yake, yule Msamaria, mtu wa kabila lisilo na thamani lakini yeye mwenyewe akawa na roho ya utu. Huko ndiko inakotokea dhana ya kisasa ya UBUNTU iliyoibuliwa na ndugu zetu wa Afrika Kusini, hata kama wao wenyewe kwa kiasi kikubwa dhana hiyo inawashinda.

Na tuwe watu, basi, badala ya kuwa binadamu tu, kwa sababu ni utu peke yake unaotutofautisha na hayawani. Utu unatutaka tuwatendee wenzetu, hata tusiowajua,  kama vile ambavyo tungependa sisi wenye tutendewe na wenzetu, hata kama hawatujui. Kumtendea wema mtu unayemjua ni jambo jema, lakini inawezekana wema huo umetokana na jinsi unavyomjua huyo unayemtendea wema.

Inawezekana huyo unayemtendea wema ni ndugu yako au rafiki yako, la sivyo usingetenda wema uliotenda. Huo ni wema wa bei kidogo, kwa sababu kwa maana moja, huo ni wema unaojitendea wewe mwenyewe. Wema unayemtendea mtu usiyemjua unayo thamani kubwa zaidi, kwa sababu hapo unatenda wema kwa ajili ya kutenda wema, na si kwa sababu ndugu yako au rafiki yako anahusika.  

Hii inatufundisha tuwe na roho ya kuwapenda watu wote na kuwasaidia. Bila shaka kama falsafa hii ingetamalaki katika jamii iliyo pana tungekuwa na watenda wema kila kona ya jamii, na wala tusingekuwa na haja ya mahubiri ya kila wikiendi ya kuhamasishana kutenda wema.

Unapita mtaani, na unashuhudia uovu ukitendeka lakini  anayetendewa uovu huo ni mtu usiyemjua, na kwa sababu humjui, unajipitia na kuendelea na hamsini zako. Umeshindwa kutenda wema. Unamkuta mtu anatenda kosa kwa makusudi, lakini kwa sababu kosa hili hakikuumizi wewe mwenyewe kwa namna yo yote ile, unaona ni jambo lisilokuhusu na unaendelea na safari yako kana kwamba hukuona jambo lo lote.

Kosa la kuwa na mitazamo kama hii ni kwamba si wewe pekee utakayefanya hivyo. Wenzako pia, katika pita-pita zao watashuhudia maovu kama lile uliloshihudia na watakaa kimya kwa sababu hayawahusu, lakini kumbe linakuhusu wewe, lakini kwa sababu jamii yenu ilikwisha kujizoeza kutokuingilia mambo yasiyowahusu, utaumia na hakuna atakayekusikia.

Watanzania tumekwisha kufikia kiasi hiki cha kutokujali. Tunawaona watu wanaumizwa kila siku, lakini kwa sababu hao wanaoumia si ndugu zetu au marafiki zetu, tunaendelea na hamsini zetu kama vile hatujaona kitu. Tunasahau kwamba na sisi tutakapokuja kupatwa na hayo, wenzetu nao hawataona tunavyoteseka. Hakuna utu unaotendeka kwa kubaguana baina ya wale wanaostahili kutendewa haki na wale wasiostahili kutendewa haki. Bima ya kweli ya w ewe kutendewa haki na watu wasiokujua ni wewe kutenda haki kwa wale usiowajua.              

Tumewaona wakuu wa polisi wakiangalia watu wanapigwa na kuumizwa, halafu wakuu hao wanatoa visingizio vya kutia kichefuchefu, mara nyingi wakiwalaumu wahenga kwamba ndio walioanzisha fujo. Mkuu kama huyo wa polisi akija kumkuta mwanaye kapigwa na kutobolewa jicho na askari polisi asiyemjua, atakuwa na ujasiri wa kumlaumu mwanaye kwa kuwa sababu au chanzo cha kujeruhiwa kwake?

Tunashuhudia watu wakikamatwa na kufunguliwa mashitaka mbali mbali ambamo vinaingizwa vipengele vya money laundering , hata katika mazingira yasiyofanana kabisa na kosa hilo. Kisa ni kwamba waendesha mashitaka wanatafuta njia ya kuhakikisha kwamba mshitakiwa hatoki nje kwa dhamana.

Halafu, kwa muda mrefu tumekuwa na utaratibu ambao sielewi ulitoka wapi, eti ofisa huyo huyo anayekushitaki ndiye pia amwambie hakimu iwapo unafaa kupewa dhamana au la! Mambo yale yale, ya riwaya za George Orwell. Huyu ndiye anashitaki, na anataka mshitakiwa afungwe, halafu ndiye anaulizwa iwapo anadhani ni sawa kwa mshitakiwa kuachiwa kwa dhamana!  Tusije kuwasingizia Wazungu kwamba ndio waliotufundisha mantiki hii. Hii ni yetu na tuliipata kule kule katika ‘collective imbecilization’ ya Seithy  Chachage.

Wakati naandika makala hii tumepata habari kwamba katika jimbo fulani la ubunge, mgombea wa chama cha upinzani ameshindwa kukabidhi fomu za kumfanya mgonbea, halafu anatangazwa mgombea wa chama tawala kwamba amepita bila kupingwa! Hivi huu si utaratbu wa kuwafanya watu wapate kichaa na hatimaye waseme, ‘liwalo na liwe!’?

Najiuliza ni kwa nini tunadhani kwamba vurugu zinazozuka katika nchi nyingine za bara la Afrika haziwezi kutokea kwetu. Wale waliokumbwa na vurugu tunazozifuatilia ni watu wenye akili kama sisi, na hawajamkosea Mungu kwa kiasi kinachozidi makosa yetu kwa Bwana Mkubwa huyo. Ni kwa nini tunadhani kwamba sisi tunayo kinga inayotufanya tuenende bila kujali mantiki, halafu tuepukane na hayo yaliyowapata wenzetu? 

Msingi wa amani ni haki, bila haki hatuwezi kuwa na amani. Aidha, haki haina tabia ya kuangalia sura ya mtu, wala kabila lake, wala dini yake. Ndiyo maana alama ya haki duniani kote ni yule mawanamama aliyefungwa kitambaa usoni; haoni. Tunapokuwa na mifumo ya kutoa haki kwa upendeleo unaotokana na kuwaangalia watu usoni hatutakuwa na haki hata chembe.

Nasema kwamba msingi wa haki zote ambazo tunadai leo ni haki ya ushiriki wa kisiasa. Bila kuwa na haki katika ushiriki katika siasa hatuwezi kubuni haki nyingine zo zote na zikawa na mashiko. Ushiriki wa kisiasa kwa raia wote unapokuwa umetengenezewa mifumo inayokubalika na watu wakairidhia, ndiyo bima ya juu kabisa ya kuondoa uwezekano wa chokochoko ndani ya jamii.

Mtawala mwenye busara ataiona hii mantiki, na kila siku atapanuwa wigo wa ushiriki huo ili asiachwe ye yote nje ya wigo wa ushiriki wa kisiasa. Mtawala asiye na busara hii atazidi kila siku kubinya hata ule wigo uliopo, huku akiongeza asilimia ya wale wanaoachwa nje ya wigo wa ushiriki. Huyo anaitakia majanga jamii yake. 

Akina Lupondije na Johnson

NI vigumu kuzungumzia vipengele vya utamaduni vinavyoathiri juhudi zetu za maendeleo bila kujali suala la imani za ushirikina katika jamii zetu. Hizi ni imani zenye nguvu kubwa inayochangia sana katika kurudisha nyuma jitihada zetu.

Katika uhusiano wa kidialektiki, imani hizi zinatokana na viwango duni vya maendeleo yetu, lakini papo imani hizi zinachangia katika kutufanya tuendelee kuwa na maendeleo duni. 

Imani hizi zinatokana na itikadi za kale za mababu na mabibi zetu, itikadi ambazo ndizo zilizokuwa dini zao halisi kabla ya jamii zetu kuingiliwa na wageni waliokuja na imani zao na kuzipandikiza miongoni mwetu.

Wazee wetu waliamini katika vitu halisi walivyoviona, na ambavyo viliwakilisha nguvu za kimungu—miti, wanyama, milima, mito, radi, upinde-wa-mvua, na kadhalika. 

Katika itikadi zao, vitu hivi vilikuwa na maana na kwa kuviabudu walipata nafuu kutokana na jambo lo lote waliloliona kama tatizo kwao kwa nyakati mbali mbali.

Kwa jinsi hii, walikuwa na miungu wa kusaidia kilimo; miungu waliosimamia uzazi; miungu walioleta mvua; miungu walioepusha shari safarini; miungu waliowalipia kisasi dhidi ya wabaya wao, na kadhalika.

Ujio wa wageni kutoka Uropa na Arabuni, ulileta imani mpya ambazo zilipata umaarufu haraka kutokana na sababu mbali mbali, ikiwa ni pamoja na ukwasi wa wageni hao na nguvu zao za kiuchumi, kiteknolojia na kadhalika. 

Kwa kuwa itikadi zetu za asili hazikuweza kushindana na zile za wageni hawa, wazee wetu walilazimika kuzihama imani zao na kuzikubali hizi mpya.

Mara nyingi itikadi za wageni hawa ziliambatana na utawala wa dola, uendeshaji wa biashara na nguvu za kivita—ambavyo  vyote vilitumika kuzididimiza imani za asili na kulazimisha ziingie mafichoni. Mbinu mbalimbali zilitumika katika kufanikisha hili.

Katika baadhi ya sehemu, kilichotumika ni nguvu za wazi. Wakubwa walitumia mtutu wa bunduki kuonyesha umahiri wa mungu wao, umahiri ambao haukuweza kuonyeshwa na mungu ye yote wa Kiafrika. 

Katika sehemu nyingine walitumia teknolojia na mazao yake, ikiwa ni pamoja na vitu vidogo vidogo visivyo na thamani, lakini ambavyo vilikuwa virojakwa wazee wetu mbumbumbu. Mahali pengine zilitumika mbinu mchanganyiko: Nguvu kidogo, viroja kidogo na mahubiri mengi.

Katika kipindi kifupi, wazee wetu walijikuta wameziacha imani zao na kukumbatia zile za wageni walioonekana mbali sana kimaendeleo. Kutokana na unyonge wao, ilibidi wazisabili imani zao. Na hivi ndivyo ilivyokuwa siku zote: Dau la mnyonge haliendi joshi. Mawazo ya mnyonge hayana thamani. Anachoamini mnyonge si hoja.

Kwa muda mrefu imani zetu za asili zilionyeshwa kwamba hazina maana mbele ya imani za wageni. Zikapigwa vita kali kweli kweli. Watu wakaambiwa kwamba imani zao ni za kishenzi. Miungu wao wakatukanwa na wakadhalilishwa. Matambiko yao yakazomewa. Majina yao yakabadilishwa, akina Lupondije, Kalimanzira, Mwakatumbula na Kisha wakaitwa Johnson, Abdullatif, Gordon na Shamsa.

Hapa, siwezi kusahau tukio moja miaka mingi iliyopita, wakati mwalimu wetu wa shule ya msingi wilyani Bukoba alipozungumza na hadhira ya watoto wote wa shuleni hapo. 

Siku hiyo mada yake ilihusu mabadiliko ya majina. Tulikuwa na watoto wengi waliokuwa na majina kama vile John Paul, Regina William, Issa Yassin, Mariam Yahaya, na kadhalika. Ujumbe wa mwalimu kwa siku hiyo ulikuwa mzito: “Wale wote wenye majina ya dini, waseme iwapo wanataka kubadili na kuandikisha majina ya kishenzi”! Jambo muhimu ni kujua kwamba mwalimu huyu alikuwa mzalendo.

Katika hali hii, imani zetu za jadi zililazimika kujificha na kufanya sherehe zake katika mahafali ya siri, zikaogopa mwanga, zikakosa hewa safi ya ujenzi wa kisasa, zikiendesha mambo yake kwa haya na tahadhari kubwa, zikavia na kudumaa.

Lakini hazikufa, washiriki wake waliendelea kuzifuata, ingawaje kwa kujificha. Leo bado maelfu kwa maelfu ya watu hapa nchini na kote katika nchi zinazoitwa ‘zinazoendelea’, wanaamini katika itikadi hizi. Hata wale wanaojiita Jeremiah na Twaha na ambao wanakwenda kanisani na kukomunika au kusujudu, ‘bado wanapita mara moja moja kupata ushauri wa fundi’ wakati maji yanapofika shingoni. 

Kwa nini? Imani ni imani. 

Msingi wake katika uyakinifu ni mwembamba mno, na mara nyingi mantiki hupewa nafasi ndogo sana. Wale waliotaka kupata majibu yakinifu kwa kila walichokisaili, waliachana kabisa na imani, wakataka kujua.

Wale waliokumbatia imani ya aina moja au nyingine, waliendelea na imani waliyoiteua au iliyoteuliwa na wazazi wao. Lakini mara wanapojikuta na maswali mengi kuliko majibu yanayopatikana katika imani zao, wanakuwa wepesi kujaribu imani nyingine; hata kama wazazi wao waliwaingiza katika imani mpya walikuwa bado wanachukua bima katika imani za kale.

Kama nilivyosema hapo juu, imani mpya zilikuja na sayansi, teknolojia, biashara na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kwa ujumla, kimantiki, kadri mtu alivyojiona ameendelea, ndivyo imani yake katika itikadi mpya ilivyoimarika, akawa Muislamu wa kweli au Mkristo wa kweli.

Wale ambao hawakuendelea kiasi hicho, walibaki katika imani zao za jadi, kwa sababu kimsingi, hali za maisha yao ya kawaida hazikuachana mno na hali zao za asili. Hii si nadharia tupu. Hali ya maisha ya wanavijiji wetu leo imebadilika kiasi gani kutoka ilivyokuwa nusu karne iliyopita?

Lakini hata wale waliojiona, au walioonekana kama walioendelea, nao hawakwenda mbali sana. Wamesoma, wana shahada, wametembea Uropa na kwingine ughaibuni, wanaishi katika majumba ya kifahari na magari yao yanatisha. Lakini hatukwenda kujifunza ustaarabu wa wenzetu, bali kununua viroja vya ustaarabu huo. Tunaishi katika makasri ya ajabu na kuendesha magari makubwa bila kuelewa teknolojia ya msingi inayotengeneza hata mkokoteni.

Kifupi, vitu hivi si vyetu; sisi ni waigizaji, sawa sawa na wanawake weusi wanaotumia mkorogo ili wawe weupe, hivyo hivyo kwa itikadi zetu mpya zilizoletwa kutoka Uropa na Arabuni. Kwa watu wengi itikadi ni mpakazo, na hawajui ni kwa nini wamejikuta katika dini hizo, hata kama baadhi yao wanasema wako tiyari kuua au kuuawa katika kuzitetea itikadi hizo.

Mwangalie Mkristo au Mwislamu “mzuri” anapokabiliwa na shida ya kweli. Inawezekana kuwa ni ugonjwa wa mwanae, au kesi inayotishia kumfunga, au ndoa yake imekwenda mrama au biashara yake imevurugika. 

Atakwenda hospitali, atamwona wakili, atatafuta ushauri-nasaha, atatafuta mshauri wa uchumi, na kadhalika, kufuatana na aina ya tatizo alilo nalo.

Kwa kuwa ni muumini pia, atakwenda kusali kanisani au msikitini. Atasoma rozari, au atavuta uradi. Atamwona padre, kasisi na sheikh kumtaka mawaidha au kumwomba amsalie mtoto wake, au awapatanishe yeye na mke au mume wake. Atafanya mambo yote anayotakiwa kufanya muumini mzuri.

Lakini yote haya yakishindikana, Mkristo au Mwislamu wetu, atakumbuka jadi yake. Atakwenda kwa ‘fundi’ ili amsaidie pale ambako kanisa au msikiti vmeshindwa kumsaidia. Haya ni mambo yanayotendeka kila siku katika jamii yetu, hata kama hatutaki kuyakubali, kwa sababu ni mambo yanayotendeka kwa kificho na siri.     

Kila ajaye ana jipya, hatuendi kokote

Katika makala yangu ya mwisho, wiki mbili zilizopita, nilionyesha jinsi ambavyo wakuu waliostaafu wanvyolalamikia mambo ambayo wao wenyewe waliyasababisha walipokuwa madarakani kwa kutotaka kusikiliza kilichokuwa kikisemwa na wengine, wakidhani kwamba maoni ya mkuu ni bora kuliko ya wale wasio na ukuu.

Marais wastaafu wawili walikuwa wametoa maoni yao kuhusu mporomoko wa viwango vya elimu, wakisema kwamba hili ni janga la taifa. Ni kweli kwamba elimu yetu imeporomoka kwa kiasi cha kutisha, kama ambavyo tafiti zetu zinavyoonyesha. Lakini hao wawili walikuwa madarakani wakati fulani, na kila aliyejaribu kuwaambia hayo ambayo wanayasema leo walimuona kama mwendawazimu, punguani, muongo au ‘mvivu wa kufikiri.’

Nachelea kufikiri kwamba mkuu tuliye naye sasa, kwa kufuata mfano wao, anaweza kuwaita hao watangulizi wake majina hayo. Natumai hatofanya hivyo bali atajifunza kutokana na kasoro zao ili naye asije akaanza kulalama baada ya kutoka madarakani kuhusu mambo ambayo alikuwa na uwezo nayo alipokuwa madarakani lakini akawabeza waliotaka kumshauri.

Tukumbushane akili: Serikali ina wajibu wa kutawala, na katika shughuli hiyo, ni serikali pekee yenye wajibu huo. Hakuna chombo kingine chenye wajibu wa, au haki ya, kutawala isipokuwa serikali. Minajili ya kufanya kazi hiyo, serikali imepewa vyombo vya utekelezaji, kama vile utawala wa raia, pamoja na asasi za kimabavu, kama vile majeshi, idara za upelelezi na ujasusi, vitengo vya makachero na wachunguzi.

Lakini, pamoja na nguvu zote hizo ilizopewa serikali kwa ukiritimba, haiwezekani serikali yo yote ikatamba kwamba ina ukiritimba wa akli, maono ama ujuzi katika mambo yote. Idadi yote ya watu waliomo serikalini katika ngazi ote ni ndogo mno, na uwezo wa kila mmoja wao kumiliki akili, maono, taarifa na weledi ni huo anaoweza kuwa nao mtu mmmoja, na uwezo wao wote ukichanganywa pamoja bado utakuwa ni kidogo ukilinganishwa na uwezo wa pamoja wa raia wa nchi husika.

Ndiyo maana ni hatari kwa watawala kudhani kwamba wanao uwezo wa utambuzi na uelewa kuwazidi wananchi wao. Na ndiyo maana, baada ya karne nyingi za mapambano baina ya matabaka hasimu, wenzetu walioendelea walitambua kwamba hawana budi kujenga mifumo na michakato inayotambua upungufu wa uwezo wa watawala, na kuweka utaratibu wa kurutubisha uwezo huo kwa kuukutanisha na uwezo unaopatikana miongoni mwa wananchi wasio na dhima ya kutawala. 

Kutokana na kutambua hivyo, wenzetu waliweka utaratibu kama vile uwakilishi katika halmashauri na mabunge ambamo wawakilishi wao walipeleka hoja zao na kuzishindanisha, maslahi ya hawa yakikinzana na maslahi ya wale, huku pande zote zikizingatia maslahi ya pamoja ya kitaifa. Miundo na  mifumo hiyo tulirithishwa na wakoloni wakati wakiondoka, na hadi sasa tunayo, hata kama tumeifanya ni kama mazindiko hasi yasiyokuwa na faida yo yote kwetu.

Lakini wenzetu wamekuwa wakiendelea na mifumo na michakato yao, ambayo wameipa uzima na kuifanya hai. Mabunge yao yanafanya kazi ya kuzikosoa, kuzielekeza na kuzidhibiti serikali zao. Halmashauri zao zinafanya vivyo hivyo. Inapofikia kwamba watawala wameonekana hawana usikivu, mabunge haya na halmashauri hizi inao uweo wa kuwaondoa madarakani.

Kwetu sisi tumebaki na mabunge na halmashauri magarasa, mapambo ambayo yanapendeza kuyaangalia na kumuonyesha mgeni, lakini huwezi kuyatuma sokoni. Ni mpangilio ulio ghali mno, lakini ambao hautuzaliii matunda tuliyotaraji.

Hata hivyo, hali kama tuliyo nayo, kimsingi siyo ya kwetu peke yetu. Wakati katika historia ya binadamu kumekuwapo na misuguano baina ya matabaka mbali mbali, au makundi mbali mbali, kila moja likipigana ili kuongeza manufaa yake, lakini  kila muhula wa mapambano hayo hulizipeleka jamii husika katika ngazi mpya juu ya pale zilipokuwa awali.

Sisi tunaelekea kuwa tofauti. Ni kama vile tunatembea kinyumenyume. Mahali ambapo tulikwisha kupitia jui ndiko tunakotaka kurejea leo. Ni mithili ya watu wazima wanaotaka kunyonya vidole, kama watoto. Hatuelekei kama watu wanaojua hatua za kihistoria walizozipitia.

Mojawapo ya matatizo yanayotukwaa ni kutokuwa na utaratibu unaoeleweka na unaoufuatwa wa kupokeana utawala (achana na uongozi kwa sasa). Alipoondoka Julius Nyerere na kumwachia urais Ali Hassan Mwinyi, kwa miaka mitano Mweinyi alionekana akifanya kazi nzuri mno, kwa sababu, kimsingi, Nyerere alikuw ahajaondoka moja kwa moja. 

Kwanza Nyerere ndiye alikuwa bado mwenyekiti wa chama-tawala. Maamuzi yote yalipitia mikononi mwachama kabla hayajatekelezwa serikalini. Lakini pia, waziri mkuu wa Mwinyi alikuwa Joseph Warioba, ambaye mtazamo wake ulifanana sana na ule wa Nyerere, hata kama alikuwa hapokei maelekezo yo yote toka kwa Mzee. Muhula wa wa pili wa Mwinyi ukaja kuwa tofauti kabisa na ule wa kwanza kwa sababu, kwanza Nyerere aliachia uenyekiti na Warioba akaondolewa kwenue uwaziri mkuu, na hapo ndipo tukaziona sura halisi za Mwinyi.

Tangu hapo tunachoshuhudia ni kila anayekuja kuja na lake, na hakuna mwendelezo way ale aliyoyakuta. Wakati mwingine wakuu wanatoa taswira kama vile utawala mpya umeingia kwa kuupindua utawala uliopita, au kama vile chama kipya (kilichokuwa upinzani) kimeingia madarakani. Kila anayeingia anaingia na timu yake ambayo lengo lake kuu ni kufutilia mbali yale yote yaliyofanywa na mtangulizi wake.

Katika awamu inayoitwa ya tano (binafsi naona awamu imekuwa ni moja tu tangu 1961), mambo mengi makuu ya ‘awamu’ ziliopita yametupwa nje, hata yale yenye manufaa ya dhahiri, kwa sababu wakuu wapya wana upendeleo kwa mambo mengine tofauti. Najiulia iwapo ‘awamu’hii itakapopita hakutakuja wengine naao wakayatupilia mbali haya tunayoyaona yakifanyika hivi sasa? Hili nitalieleza kwa kina huko mbele.

Kwa jinsi hii, hatuendi ko kote, kwa sababu hatulimbikizi matendo, ujuzi, uzoefu na manufaa; kila siku sisi ni watu wa kuanza upya. 

Itaendelea        

Oksijeni, tiba ya damu chovu

Yanawakereketa watu wengine au la. Kwa hakika ni jambo la kukatisha tamaa iwapo unaandika kila wiki na kila unaloliandika ni jambo ambalo unadhani lina umuhimu wake, lakini usipate fununu kwamba watu wamesoma yale uliyoyaandika, na ama wamefurahishwa nayo au wamekasirishwa.

Iwapo watu wamefurahishwa au wamekasirishwa, hii siyo hoja. Hoja ni kwamba wamesoma na wameelewa. Wakati mwingine napenda kupata mawazo ya wale waliokasirishwa kuliko ya wale waliofurahishwa.

Hii ni kwa sababu mara nyingi wale waliofurahishwa ni watu walio na mawazo ambayo kwa mapana yake ni sawa na yangu. Hawa hawanisaidii sana kupanua mawazo yangu, kwa sababu kile wanachokisema ndicho hicho ninachokisema mimi, ukiacha tofauti ndogo ndogo.

Mawazo yanayopingana na yangu yananikuna zaidi kwa sababu yananifungulia madirisha mapya ya fikra ambazo zinanisaidia kuona ni wapi nilipotoka au ni wapi sikufanya uchambuzi unaopasa. Hii ni elimu kubwa kwangu na kwa mtu yeyote mwingine aliye katika nafasi kama yangu.

Lakini ingeweza kuwa elimu kubwa zaidi kwa wale walio madarakani, wale waliochaguliwa na wananchi kisha wakakabidhiwa majukumu ya kutekeleza kwa niaba ya waliowachagua. Laiti hawa wangesikiliza maoni yanayotofautiana na yao, wangegundua kwamba kila siku ni siku ya elimu.

Kwa bahati mbaya hii haitokei kwetu. Nimewahi kuandika mara mbili au tatu kwamba viongozi wetu ni watu ambao wanaamini kwamba siku mtu anapopata cheo, busara zinakuja papo kwa papo. Mimi naamini kwamba uongozi ni cheo wala cheo si uongozi.

Mtu anaweza kuwa na cheo kikubwa tu, lakini kila mtu akamwona ni juha na mwingine akawa hana cheo, lakini akatambulika kama kiongozi hapo alipo. Uongozi hutokana na nguvu ya ushawishi, na wala si cheo na ofisi. Hutokea bahati kwa nadra kwamba ushawishi unaungana na cheo katika nafsi ya mtu mmoja, na hapo ndipo jamii hujihesabu kwamba ina bahati ya kupata uongozi madhubuti.

Katika sehemu iliyo kubwa ya kuwapa nafasi ya kutumia sifa hizo kwa manufaa ya jamii yao.maisha ya jamii, kuungana kwa namna hii kwa busara na cheo hakutokei. Kwa jinsi hii tunawapata viongozi wenye vyeo bila kuwa na sifa za uongozi na watu wenye sifa za uongozi ambao hawana vyeo vya 

Matokeo yake ni kwamba wenye vyeo wataendelea kuvurunda utawala wa jamii yao, wakati wale wenye sifa bila vyeo, wanalazimika kuendeleza uongozi wao kwa njia zisizo rasmi. Utawakuta katika vyuo vikuu, mitaani, vijijini, katika vyama vya hiari, katika taasisi za kidini, ndani ya vyama vya michezo, vyombo vya habari, hata katika vilabu vya pombe, na kadhalika.

Kadri mfumo wa siasa wa nchi hii unavyozidi kutawaliwa na watu wenye uwezo wa kifedha, ndivyo watu wa aina niliyoieleza hapo juu, watakavyozidi kutoweka katika uongozi rasmi na kuzidi kupatikana katika nyanja zisizo rasmi.

Hii ni kwa sababu ni watu wachache wanaoelewa vyema madhara ya mfumo wa utawala kutawaliwa na fedha watakubali kuendelea katika mfumo huo, wakati wanajua kwamba hiyo ndiyo njia ya mkato ya kuipeleka jamii katika maangamizi makubwa.

Inatubidi basi tutambue kwamba hazina ya uongozi wa jamii yetu haiko katika uongozi rasmi tu, kwa maana ya wale waliochaguliwa na ambao wamekalia vyeo na wale walioteuliwa kufanya kazi za utendaji. Nchi nzima, jamii yote pana, ni bwawa ambamo tunaweza kuvua mawazo ya busara ambayo yanaweza kutusaidia kupiga hatua.

Hii haina maana ya kupunguza umuhimu au hata heshima ya nafasi ya wale waliomo serikalini na katika taasisi nyingine za utawala, la hasha. Yamkini kwamba serikali ndiyo iliyowekwa rasmi kuongoza taifa, na lazima ichukue nafasi ya kwanza kabisa katika shughuli hii. Serikali ndiyo itakayoulizwa na wananchi au wawakilishi wao, iwapo itashindwa kutimiza wajibu wake.

Lakini haiyumkiniki kwa serikali kujitia kwamba yenyewe ndiyo iliyo na ukiritimba wa ujuzi na busara katika masuala yote yanayohusu uongozi wa nchi. Kwanza tunajua kwamba watumishi wa serikali ni wachache mno kulinganisha na wananchi waliobaki.

Pili, tunajua kwamba watu waliomo serikalini, hata vyeo vyao vingekuwa na mvuto wa aina gani, sio wenye bongo bora nchini. Kwa kweli, wengi wao wako mbali sana na adha ya kutumia ubongo kila siku. Wamo watu ndani ya serikali ambao hupata kizunguzungu kila wanapojaribu kufikiria kuhusu jambo ambalo hawajawahi kulisikia.

Si hilo tu. Kila taasisi, baada ya kuwapo kwa muda mrefu, hujijengea utamaduni wake. Hufikia mahali utamaduni huo ukawa gamba gumu kama ngozi ya faru, ambalo kazi yake ni kuikinga taasisi hiyo dhidi ya mawazo ambayo hayakuzoeleka, bila hata ya kuyapima.

Kwa njia hii, hata watu wenye akili nzuri, baada ya muda hujikuta wakigubikwa na mawazo machovu kwa sababutaasisi iliyowalea na inayowaelekeza namna ya kufikiri, imechoka kama damu isiyopata hewa ya oksijeni.

Kama wapo watu ndani ya serikali ya Tanzania wanaodhani kwamba haya ninayoyasema yanaudhi, basi na wafarijike kwa kujua kwamba hawako peke yao. Serikali nyingine duniani ziko katika hali hiyo hiyo, hasa zile zilizobaki madarakani kwa muda mrefu zikiongozwa na watu wale wale au vyama vile vile.

Mifano ya hivi karibuni katika nchi kama Muungano wa Sovieti, Mexico, Indonesia na hata Ujerumani, inaonyesha ukweli huu. Nimechukua mifano ya nchi hizi kwa sababu ni nchi zinazotofautiana sana katika miundo ya kisiasa, uchumi na utamaduni, lakini zote zinaunganishwa na uchovu wa mifumo, au vyama, au watu walioshikilia madaraka.

Bima pekee dhidi ya uchovu wa aina hii ni kuruhusu oksijeni iingie katika damu ya utawala, mawazo mapya yapenye, fikra zirutubishwe na fikra nyingine, badala ya kuziacha zikavia na kuzaa watoto taahira kutokana na kujiamini kwa muda mrefu baina ya fikra zile zile.

Hii haina maana kwamba ni lazima kubadilisha serikali, au chama kinachotawala, iwapo serikali na chama chake vinayo dainamiki ya kuweza kuruhusu kushamiri kwa mawazo mapya, ama kwa kuyapata mumo humo ndani yao, au kwa kuyachukua kutoka nje. Lakini hii inaposhindikana, na mfumo ukajikuta umevimbiwa, inakuwa hakuna suluhu, ila kubadilisha kila kitu na kuanza upya.

Hapo juu nimesema kwamba watawala wanaweza kupata hiyo oksijeni kutoka ndani ya utawala wao wenyewe au kuipata nje ya utawala wao. Hii ina maana kwamba wanaweza wakanufaika kwa kusikiliza maoni yanayotokana na upinzani, kama vile upinzani unavyoweza kunufaika kutokana na mawazo ya watawala. Vinginevyo, kazi ya upinzani ni nini?

Lakini hakuna mbadala wa maoni ya wananchi na ustawi wao. Viongozi wote wa kisiasa wanawajibika kuwasikiliza wananchi wanasema nini na kuyatia maanani mambo hayo yanayosemwa na wananchi. Hakuna oksijeni iliyo safi kuliko ile inayotokana na mawazo ya wananchi ambao ndio chimbuko la madaraka na nguvu ya watawala na wale wote wanaotarajia kuzungumza kwa niaba yao.

Utamaduni unaowafanya viongozi wa kisiasa kuamini kwamba wanajua matatizo ya wananchi kuliko wananchi wenyewe ni utamaduni ulioangamiza tawala nyingi katika historia ya binadamu. Ni utamaduni unaowafaa waliomo madarakani kwa sababu tu ya kupata maslahi ya muda, na hawajali nini kitatokea wakiisha kuondoka madarakani au kufa.

Tanzania inayo bahati ya kuwa na muundo unaoeleweka wa utawala kutoka juu hadi chini. Iwapo serikali inataka maoni ya wananchi juu ya jambo lolote lile, itayapata maoni hayo katika kipindi kifupi zaidi kuliko inavyoweza kufanya serikali ya nchi nyingine yo yote ninayoijua barani Afrika yenye ukubwa kama nchi hii.

Katika historia ya nchi hii, muundo huu ulitumika mara kadhaa kupata maoni ya wananchi. Faida zake tuliziona. Swali la kujiuliza ni, kwa nini hivi sasa, wakati tunajua kwamba tunayo matatizo mengi makubwa, tunashindwa au hatutaki kushauriana na wananchi?

Jenerali Ulimwengu

Papers aside, if it doesn’t make us better human beings, it’s no education

A smartly dressed gentleman strides over to the check-in counter at the airport, takes out his ticket and demands some service that the girl behind the desk says she cannot grant because the flight is fully booked, or something like that.

The man, with “Mr Important” written all over his nose and face, argues with the hostess for some time, and then shouts at the poor girl, ‘Do you know who I am?’ several times.

The girl switches on the public address system and calmly announces, “There is a gentleman here who does not know who he is. Could someone please come over and help him discover his identity?”

Sheepishly, the man walks away quietly, hoping no one will recognize him as the a**h***.

You must have witnessed this kind of man or woman who thinks the whole world must know who they are because they are the most intelligent, the richest, the most important … Their sense of entitlement can be nauseating.

Fela Anikulapo Kuti, the legendary Nigerian crooner had a name for them: “Shakara” in his song of the same title. When you have a small quarrel with him, he asks you, “Do you know who I am. I go beat you, you go look like you get accident. Wait till I comot dis dress. Na shakara man. He no fit do notin. Na shakara logic.”

It has become fashionable to be “shakara” in our neck of the woods, especially with people with some semblance of power or what they call “education.” You will hear people talk loudly about the “education” they possess, usually meaning they have a number of university degrees. This lack of humility frequently attacks people who are in the midst of losing an argument and who look to get out of defeat by using “shakara” tactics.

So, in recent days an honourable  minister, who I know to be very capable otherwise, gets irked by a musician who sings political songs against President John Magufuli’s government. The minister thinks the little man should stick to singing, otherwise he should start a political party and “do politics.” Somewhere along the line, the “shakara” thing comes out.

“I have so many degrees, I can’t argue with a grade seven boy. What can he tell me?”

I am sure in my mind that the minister knows the importance of giving all citizens the space within which to engage public thinking, including on political, economic and cultural issues without necessarily being politicians, that is without having to be paid salaries for being politicians, such as ministers are paid. It is called civil society, that space within which politics gets civilised, at some remove from the putrid waters of our politicians’ politics.

As for being highly educated, that must denote culture, a moulding of the body, mind and spirit of the person so that they become better human beings, and they recognise everyone’s place in societal and national discourses.

We don’t have to hold degrees all of us. Some will excel in academics, some will apply what the academics have propounded, and some will ignore all of that and go on to do their thing quite well. Such is the truth of the likes of Bill Gates, Mark Zuckerberg, Steve Jobs ….

A few years ago I rhetorically asked a group of youngsters about a Didier Drogba and a fictitious mathematics professor. If a Drogba can run as fast as Usain Bolt toward the opposing goal, all the while glancing back at his central defender with the ball he expects to be passed to him, and all the time he is watching the defence wall he must breach, and still retains the composure to “amortise” the ball with his left foot, bring it down to his right boot and get the angle at which to take it past the monkeylike goalkeeper to score … who is the mathematics savant between this Ivory Coast man and the Harvard professor of trigonometry?

How does academic intelligence deny the place and role of the psychomotor intelligence of a well-tuned body, or the emotional intelligence of someone who has learnt to deal with a wounded society that needs healing, a branch of intelligence which has been denied so many of our bookish brothers and sisters?

Most of all, education is humanity; it’s different from skilling. A dog can be taught all sorts of skills, but I have never heard of an educated dog.

Jenerali Ulimwengu is chairman of the board of the Raia Mwema newspaper and an advocate of the High Court in Dar es Salaam. E-mail: jenerali@gmail.com

Eppur si muove

WAKATI bado naendelea kujadili kuhusu ujenzi wa utamaduni wa ujasiri wa kusema ‘hapana’ hata kama anayeambiwa ni mkubwa, amejitokeza Patrick Rutabanzibwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini na Nishati, kama vile kuunga mkono niliyokuwa nikisema katika makala zangu.

Binafsi sijui kama mradi wa IPTL anaoupinga Patrick ni wa manufaa au la kwa taifa hili; sijapata wasaa wa kuudurusu vya kutosha. Inawezekana kabisa kwamba mradi huo ni wa manufaa makubwa kwa Watanzania, lakini Patrick ameshindwa kuelewa marefu na mapana yake. Inawezekana pia kwamba mradi huo haufai hata kidogo.

Hiyo si hoja yangu; hoja yangu ni kwamba kijana huyu ameweza kuwa na msimamo anaouamini na akaweza kuueleza waziwazi bila kujali sana kwamba baadhi ya wakubwa zake hawakuwa pamoja naye katika hili.

Hii peke yake inatosha, kama ambavyo nimejaribu kueleza mara kadhaa katika safu hii. Mojawapo ya matatizo yetu makubwa ni upungufu wa watu wenye tabia kama ya Patrick. Watu katika nafasi kama aliyo nayo ni waoga, wanafiki, waongo. Wakati mwingine wanakuwa waoga hata kama hakuna hatari zinazowakabili iwapo watasema wanachoamini.

Matokeo yake ni kwamba watu wanaonyesha “kukubaliana” juu ya jambo, lakini hakuna aliyelitekeleza kwa sababu angalau nusu ya wale waliojitia kulikubali hawalikubali kwa dhati, ila kwa sababu tu wakuu walitaka kuona taswira ya makubaliano hata kama maudhui hayako hivyo.

Naamini kwamba hili ni mojawapo ya matatizo makubwa yaliyoifanya nchi hii isiendelee. Hakuna njia ya kusonga mbele iwapo watu wanavuta kamba kila mtu kuelekea upande wake, alimradi hawasemi hadharani kwamba wanapingana.

Ni bora mara elfu kwa watu kuelezana waziwazi tofauti zao na kisha wakatafuta njia ya kuziondoa, badala ya kudanganyana na kisha kila kinachodaiwa kimeamuliwa kinakwamishwa kwa makusudi katika utekelezaji wake.

Aidha, ni muhimu kwa wasaidizi na washauri kuwaambia wakubwa zao kile wanachokiamini, badala ya kuwaambia kile wanachodhani wakubwa hao wanataka kukisikia. Kama mkubwa anataka kusikia yale yanayompendeza, ni bora ayarekodi kwenye kanda kisha awe anaicheza kanda hiyo ajifurahishe kila anapopata hamu ya kufanya hivyo.

Nakumbuka wakati fulani nilifanya kazi chini ya katibu mkuu aliyenipa taabu kidogo kwa sababu mara kadhaa alikataa ushauri wa madokezo niliyomwandikia katika jalada. Badala ya kunijibu kwa dokezo, alikuwa akinipigia simu kunitaka nibadilishe msimamo wa dokezo langu ili ufanane na alivyotaka yeye. 

Nilipomshauri aandike dokezo la kukataa ushauri wangu, alikataa na kuniambia niandike dokezo jingine kufuta lile la kwanza. Nilikataa kufanya hivyo kwa sababu nilielewa kwamba alichotaka kukifanya ni kukataa kubeba lawama iwapo kile alichokitaka kifanyike kingeleta matatizo. Hii ingetoa sura kwamba, kwanza sikuwa na uhakika na msimamo wangu, na pili ingeonekana kama vile uamuzi alioufanya ulitokana na ushauri wangu, jambo ambalo lisingekuwa kweli.

Hoja yangu ilikuwa ni hivi: “Bosi, nimekwisha kukupa ushauri wangu, ila kama hukukubaliana nami niandikie kwamba hukubali, kisha nipatie  maelekezo yako mahsusi  ambayo nitayatekeleza herufi kwa herufi”. 

Mara kadhaa alikataa kufanya hivyo. Siku moja katika mazungumzo yetu ya simu aliniambia, “Wewe mkurugenzi unabishana na mtu aliye juu mtini na wewe uko chini, akikukojolea je”.

Ujumbe uliobebwa na maneno hayo ulikuwa wazi kabisa. Yeye ni mkubwa na mimi ni mdogo. Nisipokubaliana na atakavyo, nikubali kwamba ataniumiza, hata kama nina haki. Hata hivyo, niliendelea kukataa kufanya alivyotaka, kwa sababu nilitaka watu watakaosoma madokezo yangu miaka mingi baadaye, wajue ni nini hasa nilikuwa nafikiria.

Sitaki kusema nini kilitokea baada ya tishio hilo la Bwana Mkubwa wa Mtini, bali inatosha kusema kwamba baada ya hapo hatukukaa pamoja kwa muda mrefu katika wizara hiyo. Lakini ukweli ni kwamba hadi leo siwezi kuyaonea aibu madokezo niliyoandika wakati wote niliofanya kazi chini yake.

Kama nilivyosema katika makala nyingine, na kama alivyosema huyo bwana hapo juu, wanaodiriki kutoa misimamo yao waziwazi, mara nyingi huumizwa kwa njia nyingi. Watacheleweshwa kupanda vyeo. Watabaguliwa, watakemewa na kubezwa mbele ya wenzao. Wanaweza hata kufukuzwa kazi.

Sijui kama Patrick ataendelea kuwa katibu mkuu katika wizara hiyo, au wizara nyingine yoyote. Wapo wengine wanaodhani msimamo wake ni kukosa heshima mbele ya wakubwa zake. Lakini angalau safari hii, msimamo wake ulifanana kidogo na ule wa Ikulu, ingawaje msimamo wa Ikulu nao haukukubalika katika sehemu nyingine za serikali. 

Nakumbusha tena, kwamba hapa sijadili ubora au ubovu wa mradi huo. Nazungumzia maadili ya kusema lile lililo rohoni. Inaelekea baadhi ya maofisa wa serikali waliketi chini ya uongozi wa Ikulu na kukubaliana juu ya namna ya kushughulikia mradi huo. Lakini walipokwenda kwenye majadiliano na Wamalaysia, wakawa na msimamo tofauti, hali inayoashiria kwamba walikuwa hawakuwaambia wenzao ukweli. 

Ni hali hiyo inayotoa taswira kwamba serikali inazungumza kwa ndimi kadhaa tofauti, na kwamba wajumbe wanapingana wao kwa wao. Si hali inayoonyesha umoja na mshikamano ndani ya serikali. 

Katika nchi za wenzetu wanaojua maadili ya utumishi, iwapo jambo unaloliamini kwa dhati kabisa linakataliwa na wenzako, na wewe unaambiwa ukalitekeleze, una chaguo: Ama ujiridhishe kwamba mawazo yako yamebadilika kutokana na ushawishi wa hoja za wenzako, au ujiuzulu, ili uwaachie wale wanaoamini kilichokubaliwa wasimamie utekelezaji wake.

Wapo watu wanaosema kwamba mtu kama huyo akijiuzulu atakwenda kula wapi? Mimi nadhani ni maadili mabovu. Kama unaogopa kwenda “kula polisi” na kwa hiyo hutaki kujiuzulu, basi fanya kazi unavyoambiwa ufanye. Hakuna uhalali wa kuendelea kuwapo na kisha ukahujumu juhudi za wenzako.

Inabidi tujenge utamaduni mpya wa kusema lile tunalofikiri, na kulisema kwa uwazi. Tujenge utamaduni wa kubishana, tena sana, lakini kwa kutoa hoja na kuzishindanisha, hii ikiwa ni njia ya kupima uzito wa hoja ili tuweze kufanya uamuzi ulio bora.

Hili haliwezekani kutendeka iwapo tunadhani kwamba mkubwa ndiye mwenye busara zote, ndiye anayejua kila kitu. Mara nyingi wajuzi wa mambo hawawi wakubwa, kwa sababu katika mazingira mengi, ukubwa huandamana na kutotaka kujua. Kwa hiyo wakubwa wasipachikwe busara wasizokuwa nazo, na wala wao wenyewe wasiruhusiwe kujipachika busara hizo.

Kisha, lazima tukumbuke kwamba mara nyingi katika historia ya binadamu, hatua kubwa za maendeleo zimetokana na watu fulani fulani waliodiriki kusema “hapana” dhidi ya hali walizozikuta na ambazo zilikuwa zimezoeleka. Niliwataja wachache katika makala ya safu hii wiki chache zilizopita. Leo napenda nichukue mfano wa mmoja wao.

Simulizi zinatueleza kwamba Galileo alipoanza kueneza nadharia yake kwamba katika mazingira ya sayari dunia ndiyo hulizunguka jua na wala si jua linaloizunguka dunia, moja kwa moja alionekana anasema maneno ya hatari mno, kwani wakati huo itikadi ya Kanisa Katoliki na imani za wanazuoni wa wakati huo, ambao walilazimika kufuata mtazamo wa Kanisa, ilikuwa kwamba jua linaizunguka dunia, kama vile tulivyoona linatokea Mashariki na kuchwelea Magharibi kila siku.

Makao makuu ya Kanisa, Vatican, yakamtaka Galileo aende huko, ili aeleze kisa cha kufanya kufuru kama hiyo. Katika usaili mrefu uliomchosha, Galileo aling’ang’ania msimamo wake kutokana na uhakika aliokuwa nao ambao ulitokana na utafiti wake.

Lakini baada ya vitisho vya kufukuzwa na kutengwa na Kanisa, na baada ya kuwa ameteseka sana na maswali ya ‘wanazuoni’ wa Vatican, Galileo alikubali kutia saini kwenye maandiko ya kutubu na kukubali kwamba dunia haizunguki bali ni jua linalozunguka. Makadinali na wakuu wengine wa Kanisa wakafurahi kwa sababu msomi huyu mkubwa alikuwa ‘katubu’.

Hata hivyo, baada ya haya yote, wakati akiondoka kurudi nyumbani kwake, Galileo alisikika akisema kwa sauti ya unyonge na uchovu mkubwa: Eppur si muove! (Hata hivyo inazunguka tu!)

Akina Lupondije na Johnson

Ni vigumu kuzungumzia vipengele vya utamaduni vinavyoathiri juhudi zetu za maendeleo bila kujali suala la imani za ushirikina katika jamii zetu. Hizi ni imani zenye nguvu kubwa inayochangia sana katika kurudisha nyuma jitihada zetu.

Katika uhusiano wa kidialektiki, imani hizi zinatokana na viwango duni vya maendeleo yetu, lakini papo imani hizi zinachangia katika kutufanya tuendelee kuwa na maendeleo duni. 

Imani hizi zinatokana na itikadi za kale za mababu na mabibi zetu, itikadi ambazo ndizo zilizokuwa dini zao halisi kabla ya jamii zetu kuingiliwa na wageni waliokuja na imani zao na kuzipandikiza miongoni mwetu.

Wazee wetu waliamini katika vitu halisi walivyoviona, na ambavyo viliwakilisha nguvu za kimungu—miti, wanyama, milima, mito, radi, upinde-wa-mvua, na kadhalika. 

Katika itikadi zao, vitu hivi vilikuwa na maana na kwa kuviabudu walipata nafuu kutokana na jambo lo lote waliloliona kama tatizo kwao kwa nyakati mbali mbali.

Kwa jinsi hii, walikuwa na miungu wa kusaidia kilimo; miungu waliosimamia uzazi; miungu walioleta mvua; miungu walioepusha shari safarini; miungu waliowalipia kisasi dhidi ya wabaya wao, na kadhalika.

Ujio wa wageni kutoka Uropa na Arabuni, ulileta imani mpya ambazo zilipata umaarufu haraka kutokana na sababu mbali mbali, ikiwa ni pamoja na ukwasi wa wageni hao na nguvu zao za kiuchumi, kiteknolojia na kadhalika. 

Kwa kuwa itikadi zetu za asili hazikuweza kushindana na zile za wageni hawa, wazee wetu walilazimika kuzihama imani zao na kuzikubali hizi mpya.

Mara nyingi itikadi za wageni hawa ziliambatana na utawala wa dola, uendeshaji wa biashara na nguvu za kivita—ambavyo  vyote vilitumika kuzididimiza imani za asili na kulazimisha ziingie mafichoni. Mbinu mbalimbali zilitumika katika kufanikisha hili.

Katika baadhi ya sehemu, kilichotumika ni nguvu za wazi. Wakubwa walitumia mtutu wa bunduki kuonyesha umahiri wa mungu wao, umahiri ambao haukuweza kuonyeshwa na mungu ye yote wa Kiafrika. 

Katika sehemu nyingine walitumia teknolojia na mazao yake, ikiwa ni pamoja na vitu vidogo vidogo visivyo na thamani, lakini ambavyo vilikuwa virojakwa wazee wetu mbumbumbu. Mahali pengine zilitumika mbinu mchanganyiko: Nguvu kidogo, viroja kidogo na mahubiri mengi.

Katika kipindi kifupi, wazee wetu walijikuta wameziacha imani zao na kukumbatia zile za wageni walioonekana mbali sana kimaendeleo. Kutokana na unyonge wao, ilibidi wazisabili imani zao. Na hivi ndivyo ilivyokuwa siku zote: Dau la mnyonge haliendi joshi. Mawazo ya mnyonge hayana thamani. Anachoamini mnyonge si hoja.

Kwa muda mrefu imani zetu za asili zilionyeshwa kwamba hazina maana mbele ya imani za wageni. Zikapigwa vita kali kweli kweli. Watu wakaambiwa kwamba imani zao ni za kishenzi. Miungu wao wakatukanwa na wakadhalilishwa. Matambiko yao yakazomewa. Majina yao yakabadilishwa, akina Lupondije, Kalimanzira, Mwakatumbula na Kisha wakaitwa Johnson, Abdullatif, Gordon na Shamsa.

Hapa, siwezi kusahau tukio moja miaka mingi iliyopita, wakati mwalimu wetu wa shule ya msingi wilyani Bukoba alipozungumza na hadhira ya watoto wote wa shuleni hapo. 

Siku hiyo mada yake ilihusu mabadiliko ya majina. Tulikuwa na watoto wengi waliokuwa na majina kama vile John Paul, Regina William, Issa Yassin, Mariam Yahaya, na kadhalika. Ujumbe wa mwalimu kwa siku hiyo ulikuwa mzito: “Wale wote wenye majina ya dini, waseme iwapo wanataka kubadili na kuandikisha majina ya kishenzi”! Jambo muhimu ni kujua kwamba mwalimu huyu alikuwa mzalendo.

Katika hali hii, imani zetu za jadi zililazimika kujificha na kufanya sherehe zake katika mahafali ya siri, zikaogopa mwanga, zikakosa hewa safi ya ujenzi wa kisasa, zikiendesha mambo yake kwa haya na tahadhari kubwa, zikavia na kudumaa.

Lakini hazikufa, washiriki wake waliendelea kuzifuata, ingawaje kwa kujificha. Leo bado maelfu kwa maelfu ya watu hapa nchini na kote katika nchi zinazoitwa ‘zinazoendelea’, wanaamini katika itikadi hizi. Hata wale wanaojiita Jeremiah na Twaha na ambao wanakwenda kanisani na kukomunika au kusujudu, ‘bado wanapita mara moja moja kupata ushauri wa fundi’ wakati maji yanapofika shingoni. 

Kwa nini? Imani ni imani. 

Msingi wake katika uyakinifu ni mwembamba mno, na mara nyingi mantiki hupewa nafasi ndogo sana. Wale waliotaka kupata majibu yakinifu kwa kila walichokisaili, waliachana kabisa na imani, wakataka kujua.

Wale waliokumbatia imani ya aina moja au nyingine, waliendelea na imani waliyoiteua au iliyoteuliwa na wazazi wao. Lakini mara wanapojikuta na maswali mengi kuliko majibu yanayopatikana katika imani zao, wanakuwa wepesi kujaribu imani nyingine; hata kama wazazi wao waliwaingiza katika imani mpya walikuwa bado wanachukua bima katika imani za kale.

Kama nilivyosema hapo juu, imani mpya zilikuja na sayansi, teknolojia, biashara na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kwa ujumla, kimantiki, kadri mtu alivyojiona ameendelea, ndivyo imani yake katika itikadi mpya ilivyoimarika, akawa Muislamu wa kweli au Mkristo wa kweli.

Wale ambao hawakuendelea kiasi hicho, walibaki katika imani zao za jadi, kwa sababu kimsingi, hali za maisha yao ya kawaida hazikuachana mno na hali zao za asili. Hii si nadharia tupu. Hali ya maisha ya wanavijiji wetu leo imebadilika kiasi gani kutoka ilivyokuwa nusu karne iliyopita?

Lakini hata wale waliojiona, au walioonekana kama walioendelea, nao hawakwenda mbali sana. Wamesoma, wana shahada, wametembea Uropa na kwingine ughaibuni, wanaishi katika majumba ya kifahari na magari yao yanatisha. Lakini hatukwenda kujifunza ustaarabu wa wenzetu, bali kununua viroja vya ustaarabu huo. Tunaishi katika makasri ya ajabu na kuendesha magari makubwa bila kuelewa teknolojia ya msingi inayotengeneza hata mkokoteni.

Kifupi, vitu hivi si vyetu; sisi ni waigizaji, sawa sawa na wanawake weusi wanaotumia mkorogo ili wawe weupe, hivyo hivyo kwa itikadi zetu mpya zilizoletwa kutoka Uropa na Arabuni. Kwa watu wengi itikadi ni mpakazo, na hawajui ni kwa nini wamejikuta katika dini hizo, hata kama baadhi yao wanasema wako tiyari kuua au kuuawa katika kuzitetea itikadi hizo.

Mwangalie Mkristo au Mwislamu “mzuri” anapokabiliwa na shida ya kweli. Inawezekana kuwa ni ugonjwa wa mwanae, au kesi inayotishia kumfunga, au ndoa yake imekwenda mrama au biashara yake imevurugika. 

Atakwenda hospitali, atamwona wakili, atatafuta ushauri-nasaha, atatafuta mshauri wa uchumi, na kadhalika, kufuatana na aina ya tatizo alilo nalo.

Kwa kuwa ni muumini pia, atakwenda kusali kanisani au msikitini. Atasoma rozari, au atavuta uradi. Atamwona padre, kasisi na sheikh kumtaka mawaidha au kumwomba amsalie mtoto wake, au awapatanishe yeye na mke au mume wake. Atafanya mambo yote anayotakiwa kufanya muumini mzuri.

Lakini yote haya yakishindikana, Mkristo au Mwislamu wetu, atakumbuka jadi yake. Atakwenda kwa ‘fundi’ ili amsaidie pale ambako kanisa au msikiti vmeshindwa kumsaidia. Haya ni mambo yanayotendeka kila siku katika jamii yetu, hata kama hatutaki kuyakubali, kwa sababu ni mambo yanayotendeka kwa kificho na siri.