NI vigumu kuzungumzia vipengele vya utamaduni vinavyoathiri juhudi zetu za maendeleo bila kujali suala la imani za ushirikina katika jamii zetu. Hizi ni imani zenye nguvu kubwa inayochangia sana katika kurudisha nyuma jitihada zetu.

Katika uhusiano wa kidialektiki, imani hizi zinatokana na viwango duni vya maendeleo yetu, lakini papo imani hizi zinachangia katika kutufanya tuendelee kuwa na maendeleo duni. 

Imani hizi zinatokana na itikadi za kale za mababu na mabibi zetu, itikadi ambazo ndizo zilizokuwa dini zao halisi kabla ya jamii zetu kuingiliwa na wageni waliokuja na imani zao na kuzipandikiza miongoni mwetu.

Wazee wetu waliamini katika vitu halisi walivyoviona, na ambavyo viliwakilisha nguvu za kimungu—miti, wanyama, milima, mito, radi, upinde-wa-mvua, na kadhalika. 

Katika itikadi zao, vitu hivi vilikuwa na maana na kwa kuviabudu walipata nafuu kutokana na jambo lo lote waliloliona kama tatizo kwao kwa nyakati mbali mbali.

Kwa jinsi hii, walikuwa na miungu wa kusaidia kilimo; miungu waliosimamia uzazi; miungu walioleta mvua; miungu walioepusha shari safarini; miungu waliowalipia kisasi dhidi ya wabaya wao, na kadhalika.

Ujio wa wageni kutoka Uropa na Arabuni, ulileta imani mpya ambazo zilipata umaarufu haraka kutokana na sababu mbali mbali, ikiwa ni pamoja na ukwasi wa wageni hao na nguvu zao za kiuchumi, kiteknolojia na kadhalika. 

Kwa kuwa itikadi zetu za asili hazikuweza kushindana na zile za wageni hawa, wazee wetu walilazimika kuzihama imani zao na kuzikubali hizi mpya.

Mara nyingi itikadi za wageni hawa ziliambatana na utawala wa dola, uendeshaji wa biashara na nguvu za kivita—ambavyo  vyote vilitumika kuzididimiza imani za asili na kulazimisha ziingie mafichoni. Mbinu mbalimbali zilitumika katika kufanikisha hili.

Katika baadhi ya sehemu, kilichotumika ni nguvu za wazi. Wakubwa walitumia mtutu wa bunduki kuonyesha umahiri wa mungu wao, umahiri ambao haukuweza kuonyeshwa na mungu ye yote wa Kiafrika. 

Katika sehemu nyingine walitumia teknolojia na mazao yake, ikiwa ni pamoja na vitu vidogo vidogo visivyo na thamani, lakini ambavyo vilikuwa virojakwa wazee wetu mbumbumbu. Mahali pengine zilitumika mbinu mchanganyiko: Nguvu kidogo, viroja kidogo na mahubiri mengi.

Katika kipindi kifupi, wazee wetu walijikuta wameziacha imani zao na kukumbatia zile za wageni walioonekana mbali sana kimaendeleo. Kutokana na unyonge wao, ilibidi wazisabili imani zao. Na hivi ndivyo ilivyokuwa siku zote: Dau la mnyonge haliendi joshi. Mawazo ya mnyonge hayana thamani. Anachoamini mnyonge si hoja.

Kwa muda mrefu imani zetu za asili zilionyeshwa kwamba hazina maana mbele ya imani za wageni. Zikapigwa vita kali kweli kweli. Watu wakaambiwa kwamba imani zao ni za kishenzi. Miungu wao wakatukanwa na wakadhalilishwa. Matambiko yao yakazomewa. Majina yao yakabadilishwa, akina Lupondije, Kalimanzira, Mwakatumbula na Kisha wakaitwa Johnson, Abdullatif, Gordon na Shamsa.

Hapa, siwezi kusahau tukio moja miaka mingi iliyopita, wakati mwalimu wetu wa shule ya msingi wilyani Bukoba alipozungumza na hadhira ya watoto wote wa shuleni hapo. 

Siku hiyo mada yake ilihusu mabadiliko ya majina. Tulikuwa na watoto wengi waliokuwa na majina kama vile John Paul, Regina William, Issa Yassin, Mariam Yahaya, na kadhalika. Ujumbe wa mwalimu kwa siku hiyo ulikuwa mzito: “Wale wote wenye majina ya dini, waseme iwapo wanataka kubadili na kuandikisha majina ya kishenzi”! Jambo muhimu ni kujua kwamba mwalimu huyu alikuwa mzalendo.

Katika hali hii, imani zetu za jadi zililazimika kujificha na kufanya sherehe zake katika mahafali ya siri, zikaogopa mwanga, zikakosa hewa safi ya ujenzi wa kisasa, zikiendesha mambo yake kwa haya na tahadhari kubwa, zikavia na kudumaa.

Lakini hazikufa, washiriki wake waliendelea kuzifuata, ingawaje kwa kujificha. Leo bado maelfu kwa maelfu ya watu hapa nchini na kote katika nchi zinazoitwa ‘zinazoendelea’, wanaamini katika itikadi hizi. Hata wale wanaojiita Jeremiah na Twaha na ambao wanakwenda kanisani na kukomunika au kusujudu, ‘bado wanapita mara moja moja kupata ushauri wa fundi’ wakati maji yanapofika shingoni. 

Kwa nini? Imani ni imani. 

Msingi wake katika uyakinifu ni mwembamba mno, na mara nyingi mantiki hupewa nafasi ndogo sana. Wale waliotaka kupata majibu yakinifu kwa kila walichokisaili, waliachana kabisa na imani, wakataka kujua.

Wale waliokumbatia imani ya aina moja au nyingine, waliendelea na imani waliyoiteua au iliyoteuliwa na wazazi wao. Lakini mara wanapojikuta na maswali mengi kuliko majibu yanayopatikana katika imani zao, wanakuwa wepesi kujaribu imani nyingine; hata kama wazazi wao waliwaingiza katika imani mpya walikuwa bado wanachukua bima katika imani za kale.

Kama nilivyosema hapo juu, imani mpya zilikuja na sayansi, teknolojia, biashara na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kwa ujumla, kimantiki, kadri mtu alivyojiona ameendelea, ndivyo imani yake katika itikadi mpya ilivyoimarika, akawa Muislamu wa kweli au Mkristo wa kweli.

Wale ambao hawakuendelea kiasi hicho, walibaki katika imani zao za jadi, kwa sababu kimsingi, hali za maisha yao ya kawaida hazikuachana mno na hali zao za asili. Hii si nadharia tupu. Hali ya maisha ya wanavijiji wetu leo imebadilika kiasi gani kutoka ilivyokuwa nusu karne iliyopita?

Lakini hata wale waliojiona, au walioonekana kama walioendelea, nao hawakwenda mbali sana. Wamesoma, wana shahada, wametembea Uropa na kwingine ughaibuni, wanaishi katika majumba ya kifahari na magari yao yanatisha. Lakini hatukwenda kujifunza ustaarabu wa wenzetu, bali kununua viroja vya ustaarabu huo. Tunaishi katika makasri ya ajabu na kuendesha magari makubwa bila kuelewa teknolojia ya msingi inayotengeneza hata mkokoteni.

Kifupi, vitu hivi si vyetu; sisi ni waigizaji, sawa sawa na wanawake weusi wanaotumia mkorogo ili wawe weupe, hivyo hivyo kwa itikadi zetu mpya zilizoletwa kutoka Uropa na Arabuni. Kwa watu wengi itikadi ni mpakazo, na hawajui ni kwa nini wamejikuta katika dini hizo, hata kama baadhi yao wanasema wako tiyari kuua au kuuawa katika kuzitetea itikadi hizo.

Mwangalie Mkristo au Mwislamu “mzuri” anapokabiliwa na shida ya kweli. Inawezekana kuwa ni ugonjwa wa mwanae, au kesi inayotishia kumfunga, au ndoa yake imekwenda mrama au biashara yake imevurugika. 

Atakwenda hospitali, atamwona wakili, atatafuta ushauri-nasaha, atatafuta mshauri wa uchumi, na kadhalika, kufuatana na aina ya tatizo alilo nalo.

Kwa kuwa ni muumini pia, atakwenda kusali kanisani au msikitini. Atasoma rozari, au atavuta uradi. Atamwona padre, kasisi na sheikh kumtaka mawaidha au kumwomba amsalie mtoto wake, au awapatanishe yeye na mke au mume wake. Atafanya mambo yote anayotakiwa kufanya muumini mzuri.

Lakini yote haya yakishindikana, Mkristo au Mwislamu wetu, atakumbuka jadi yake. Atakwenda kwa ‘fundi’ ili amsaidie pale ambako kanisa au msikiti vmeshindwa kumsaidia. Haya ni mambo yanayotendeka kila siku katika jamii yetu, hata kama hatutaki kuyakubali, kwa sababu ni mambo yanayotendeka kwa kificho na siri.     

Leave a comment